Kongamano la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu za soka
limefanyika Jumamosi Oktoba 22, 2016 kwenye ukumbi wa Uwanja Mkuu wa
Taifa, Dar es Salaam.
Kongamano hilo lililoandaliwa na chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzani (TASWA) lilishirikisha wadau zaidi ya 60
nchini.
Kituo cha televisheni cha Azam kilionesha live (mubashara) kongamano hilo huku wajumbe wakikubaliana masuala kumi ya msingi.
Kwanza wajumbe walikubali kuwa kuna umuhimu wa kufanya
mabadiliko sasa kwa sababu muundo unaotumika kuendesha klabu za soka una
matatizo mengi.
Pili iliamuliwa klabu zijiandae vya kutosha kukaribisha
mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na kuboresha utawala bora (governance)
kwenye uendeshaji wa klabu.
Tatu mifumo yetu kama nchi inawezesha klabu kuwa na aina
nyingi za mifumo ya kiuendeshaji hivyo wanachama waelimishwe kwa kina
kuhusu mifumo hiyo ili wachague ulio bora zaidi kwa manufaa ya klabu
zao.
Nne ili mabadiliko haya yafanyike kwa haki, inatakiwa
wamiliki wa timu hizi (wanachama) waelimishwe vya kutosha juu ya
thamani yao ili wajitambue. Kwamba thamani ya klabu kubwa nchini haiwezi
kulinganishwa na kiasi cha fedha kinachotolewa na wawekezaji hivyo
wanachama wasiingie kwenye mabadiliko wakiwa wanyonge kwa sababu wao
ndio wana mtaji mkubwa kuliko hela zinazoletwa kwa ajili ya uwekezaji.
Tano mabadiliko haya hayawezi kufanywa na wanachama na
wawekezaji pekee bila kuishirikisha serikali. Hivyo klabu zinapojipanga
kwa mabadiliko haya zihakikishe zinashirikisha serikali na Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF).
Sita mabadiliko haya yasifanywe kishabiki bali yafanywe
kitaalamu ili kutengeneza msingi Imara utakaoepusha migogoro hapo
baadaye.
Saba kuelekea mabadiliko haya, hasa katika kipindi hiki
ambacho uelewa wa wanachama ni mdogo, serikali inatakiwa kulinda maslahi
ya walio wengi kwa kuingilia kati pale inapoona kuna mwelekeo wa kuwa
na mabadiliko yanayominya maslahi ya walio wengi.
Nane mpira ni biashara ya kipekee ambayo mafanikio yake
yanategemea jinsi washindani wanavyoshirikiana. Hivyo kuelekea
mabadiliko haya wanatakiwa watumike wataalamu wa biashara ya mpira ili
klabu zinapobadilika ziweke misingi itakayokubaliana na biashara ya
soka.
Tisa klabu zinao wajibu wa kulinda hadhi zake (brand) kwa
sababu eneo hilo ndio msingi wa biashara ya mpira. Hivyo klabu
zinapoelekea kwenye mabadiliko, lazima zizingatie hadhi zao
zinalindwaje.
Kumi Chama cha Waandishi wa Habari na Michezo kiliombwa
kufanya makongamao zaidi hasa kuhusiana na aina ya mabadiliko ambayo
klabu zinaweza kuingia kwa sababu inaonekana wanachama ambao ndio
wamiliki wa klabu hizi hawana uelewa wa kutosha hivyo inawapunguzia wigo
wa kuchagua aina ya mabadiliko.
SHIJA RICHARD
KATIBU WA SEKRETARIETI
KONGAMANO LA MABADILIKO YA UENDESHAJI WA KLABU ZA SOKA
Oktoba 24, 2016.
…………………………………………..
TAARIFA KAMILI
UFUNGUZI
Kongamano lilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo
la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kiganja aliwataka wajumbe kujadili hoja badala ya watu au
timu. Alisisitiza wajumbe wajadili mifumo na aina ya mabadiliko ambayo
klabu hizi zinaweza kuelekea.
Pia aliwataka TASWA kuhakikisha Waandishi wake wanaripoti taarifa zenye weledi na zenye manufaa kwa familia ya wana michezo.
Aliongeza TASWA iunde kamati ya maadili kwa ajili ya kuwawajibisha wanachama ambao wanaenda kinyume cha maadili.
WACHANGIAJI
PROFESA PROSPER NGOWI- Chuo Kikuu cha Mzumbe
Katika mada yake, Profesa anasema wanachama na wadau kwa
ujumla hawatakiwi kuogopa kufanya mabadiliko au kubadilisha namna ya
kuendesha vitu kwa sababu hilo ni jambo la kawaida.
Hata hivyo akadokeza kuwa wanachama wa Simba na Yanga
hawapaswi kuwa wanyonge kuelekea kwenye mabadiliko hayo kwa sababu mtaji
wao ni mkubwa kuliko pesa zinazoletwa na wafadhili.
“….(Wanachama) Mtaji wao mkubwa pengine sio pesa. Mtaji wao
mkubwa ni majina yaani brand ya timu hizi. Mtaji mwingine ni historia
ndefu ya timu hizi ya zaidi ya miaka 80 na ‘fan base’ kubwa sana. Pia
vikombe ambazo timu hizi zimeshida ni mtaji mkubwa sana katka meza ya
majadiliano.
Hii ni mitaji ambayo thamani yake ni kubwa kuliko pesa. Kwa
hiyo wenye timu hizi hawapaswi kuwa wanyonge kifedha mbele ya
wawekezaji. Thamani ya mitaji hii hasa brand ni kubwa kuliko pesa.”
Aliendelea kueleza, “Lazima waelewe kama wanakodisha timu
hizi, wanatoa na kupokea masharti gani? Hawapaswi kupokea tuu bali nao
watoe masharti. Waamue wanawakilishwa vipi katika uendeshaji wa timu
hizi katika nyanja zote? Brand ya timu hizi zinalindwa vipi? Ni muhimu
pia kujua kuwa kama mwekezaji atataka muda mrefu wa mkataba, Lazima
wenye timu wawe na muda na nafasi ya kufanya marekebisho ktk makubaliano
baada ya muda fulani, mfano miaka miwili au mitatu badala ya kusubiri
hadi mwisho wa mkataba, mfano miaka 10”, anasema Profesa Ngowi ambaye ni
mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara.
Profesa Ngowi anasisitiza kuwa kwa mtazamo wa kiuchumi na
kibiashara mabadiliko ni jambo la kawaida na halipaswi kuonekana la
ajabu.
“Jambo hilo linapaswa kuwa la kawaida kwa yeyote
anayependa. Hakuna sababu ya kuogopa kufanya mabadiliko au namna ya
kufanya mambo” anasema Profesa Ngowi.
Anaendelea kueleza jambo la msingi katika mabadiliko hayo
ni pande zinazohusika hasa wanachama ambao ni wamiliki wa klabu kujua ni
kipi wanachokitaka.
“Inavyoonekana wanachotaka ni hali nzuri ya kiuchumi ya
timu zao. Sio jambo baya. Wawekezaji nao wanataka maslahi ya kiuchumi
nalo sio jambo baya hata kidogo,” anasema Profesa Ngowi.
PATRIC MUSUSA – MENEJA WA MASOKO NA MIRADI KUTOKA SOKO LA HISA DSM (DSE)
Mususa anasema klabu zinapotaka kuelekea kwenye mabadiliko
hasa kwa matarajio ya kuingia kwenye soko la hisa, kwanza zihakikishe
zinabadilisha mifumo yao iliyopo sasa ili iendane na mahitaji ya soko la
hisa.
Anasema lazima zisajiliwe kuwa kampuni na Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA) na pia ziandae taarifa za fedha.
Lazima zitatakiwa kuwa na Bodi ya Wakurugenzi (BOD) watakaochaguliwa na wanahisa ambao ni wanachama wamiliki wa klabu hizo.
Kila mwanahisa atastahili kupata gawio la faida pale
kampuni (klabu) yao itakapotengeneza faida na atakuwa huru kuuza hisa
yake kama anataka kuachanana na umiliki katika klabu hiyo.
ANGETILE OSIAH, KATIBU MKUU WA ZAMANI WA TFF
Angetile anasema klabu zikihitaji kubadilisha mifumo yao
zinatakiwa kuzingatia utawala bora kwa kutofautisha majukumu
sekretarieti na taasisi nyingine zilizopo ndani ya klabu.
Anasema ulimwengu wa sasa mchezaji ni rasilimali(asset)
inayothaminishwa kwa fedha kwenye vitabu vya hesabu hivyo klabu lazima
iwe na wataalamu watakaoweza kukabiliana na changamoto hizo za utaalamu
na nyinginezo.
Anasema klabu lazima ziwe na kurugenzi za uendeshaji,
habari, biashara, sheria, fedha na masoko na ziajiri wataalamu kwa ajili
ya kuendesha shughuli hizi. Kurugenzi hizo zinahitaji wataalamu kama
waliopo kwenye taasisi nyingine za serikali na makampuni binafsi.
Anaongeza kuwa uendeshaji wa klabu lazima uzingatie utawala
bora kwa kuzipa Uhuru na mipaka ya kazi taasisi au idara zote zilizopo
ndani ya klabu.
Anawakumbusha wadau kurejea azimio la Bagamoyo ambapo
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilileta utaratibu wa kutoa
leseni kwa klabu zilizotimiza mashari.
Anasema masharti yanayotajwa yakiwemo kuwa na utawala bora,
timu za vijana n.k kama yatazingatiwa, klabu nitakuwa katika nafasi
nzuri ya kuchagua mfumo wa kujiendesha kama ni wa wanachama au wanahisa.
CHARLES NDAKI, Mtaalam wa Masuala ya Masoko
Ndaki anasema jina la timu (brand) ni rasilimali muhimu
inayitakiwa kutunzwa na kuendelezwa kwa sababu ndio msingi wa biashara
iliyopo katika soka.
Anasema klabu zinatakiwa kuweka mikakati ya kujipa upekee
ili kujitofautisha na wengine kwa lengo la kutumia vizuri jina lake
kibiashara.
Anasema kwa kufanya hivyo klabu itakuwa na wigo mpana wa
wanachama na mashabiki (fun base) NA hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa
kufanya biashara kupitia jina la klabu.
MICHAEL WAMBURA – KATIBU WA ZAMANI WA TFF
Wambura anasema serikali ndio inayoweza kulinda maslahi ya
wengi katika mabadiliko haya hivyo watumie vyombo vyake kuhakikisha
yanafanyika mabadiliko yenye maslahi kwa walio wengi.
Anasema ni vyema mabadiliko yakafanyika kwa kuzingatia
Sheria za nchi, TFF, CAF na FIFA hivyo aliviomba vyombo vinavyohusika,
TFF, BMT na Wizara kuhakikisha zinawezesha mabadiliko haya kwa manufaa
ya klabu, wanachama, wawekezaji na sekta ya michezo kwa ujumla.
HENRY TANDAU
MKUFUNZI WA FIFA
Anasema wadau katika mabadiliko haya lazima wajifunze mifumo minne ya kuendesha soka kablaya kuelekea mabadiliko
Anaongeza tatizo kubwa la wadau wa michezo hawapendo kujifunza wanaendesha klabu kwa mazoea.
Anasema biashara ya mpira ni ya aina yake kwa sababu ili
ufanikiwe inahitaji ushirikoane na mshindani wako. Kutokana na upekee
huo, biashara hii inatakiwa kuendeshwa na wataalamu wenye weledi nayo.
Anasema Azimio la Bagamoyo ndio lilitakiwa kuwa msingi
mkubwa wa mabadiliko kwa sababu limeanisha vitu vingi vizuri ambavyo
havijafanyiwa kazi.
Anaongeza kuwa japo tumechelewa lakini tulipofika tungeanza na Azimio la Bagamoyo kuelekea kwenye mabadiliko ya kweli.
JAMAL RWAMBOW, MJUMBE WA BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA BMT
Anasema mabadiliko haya hawawezi kufanyika bila
kuishirikisha serikali. “Itakuwa ni kujidanganya kuamini kwamba
wawekezaji na wanachama wanaweza kufanya mabadiliko haya bila
kuishirikosha serikali kwa sababu serikali ndio baba” anasema Rwambol.
Alitoa mwito kwa wadau kuishirikisha serikali na hasa
kufuata maelekezo yaliyotolewa na BMT kuhusiana na utaratibu wa kufanya
mabadiliko hayo kama klabu zi nataka kuelekea huko.
Mwishowe Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliahidi kwamba
chama chake kitashirkiana wadau mbali mbali kuhakikisha makongamano kama
hayo yanafanyika Mara kwa mara ili kutoa fursa kwa wadau ya kujifunza.